MAKALA::Sophia; CCM's ' Old Good Girl' Anatufundisha Nini? | furahia.newz
Breaking News
Loading...

MAKALA::Sophia; CCM's ' Old Good Girl' Anatufundisha Nini?

Habari Kubwa Kisiasa Wiki Hii:
Sophia; CCM's ' Old Good Girl' Anatufundisha Nini?

Ndugu zangu,

Bila shaka, Sophia Simba ni moja ya habari kubwa kisiasa katika juma lililomalizika. Niliziona ishara za Sophia kufanya kama alivyofanya. Niliandika kwenye ukurasa wangu wa fb, na ikawa hivyo.

Sophia Simba kafukuzwa uanachama CCM na kabaki mkereketwa wa chama. Hilo neno mkereketwa linadhihirisha kuwa Sophia ni mwanasiasa. Kwamba alikerwa, akafanya makosa kwa chama, kaadhibiwa, kakubali adhabu na kubaki mkereketwa.

Wanahabari walipomfuata, hakuwakimbia, alijua cha kuwaambia, kwa vile kilitoka moyoni mwake.

Sophia hakuondoka na Lowassa kwa kuwa alijua, kuwa alikokwenda Lowassa siko alikolelewa na kukulia. Angekwenda asikokujua.

Sophia ameonyesha pia ukomavu kwa kukiri kitendo alichokifanya Dodoma mwaka jana ni makosa. Kwamba adhabu aliyopewa anatahili. Ushujaa wa Sophia utatokea kwenye hili. Wakati utatwambia.

Nilipoandika kuwa Sophia hatoondoka CCM niliamini hivyo kwa kurejea historia. Siku zote naandika, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri.

Historia inatuambia, kuwa kuongoza Jumuiya ya Wanawake ni heshima kubwa katika nchi yenye vyama aina ya TANU na baadae CCM. Sophia aliaminika na Chama chake kwa vile ameingia kwenye chama tangu usichana wake, mwaka 1971. Sophia amekuzwa kwenye utamaduni wa TANU na CCM. Amelelewa kwenye misingi ya kiitikadi. Hata baada ya kufukuzwa uanachama, akiongea na watangazaji wa habari, tumeona, kuwa rhetoriki, kwa maana namna ya uzungumzaji wa Sophia, ni wa Ki-TANUTANU na Ki- CCMCCM.

Sophia anajua nguvu za chama tawala Afrika, na hususan Chama cha Kiitikadi- Ideology Party. Sophia sio tu amesoma habari zao, amekutana na kufundwa na akina mama wa shoka kupata kutokea nchi, ni wanawake aina ya Bibi Titi Mohammed na Sophia Kawawa. Wawili hao wamekuwa viongozi kwenye jumuiya ya wanawake TANU na CCM kitaifa.

Wawili hao wamepata kutofautiana na wenyeviti wao, lakini, hawakupata kuhama chama chao. Mmoja wao alipata hata kutiwa gerezani. Na alipotoka akakaa kimya hadi kuanza kuitwa kwenye shughuli za chama miaka ya 80.

Bibi Titi Mohammed na Sophia Kawawa wote wana mitaa iliyoitwa kwa majina yao kwenye Jiji la Dar es Salaam.

Yumkini, Sophia, CCM ' Old Good Girl', aliteleza kisiasa, nani asiyeteleza?

Maggid Mjengwa.

About Author
  • mwana habari Read More