Maoni Mazito ya Mbowe Kuhusu Madaktari 500 Kwenda Kenya | furahia.newz
Breaking News
Loading...

Maoni Mazito ya Mbowe Kuhusu Madaktari 500 Kwenda Kenya

Serikali imetangaza kuwa iko tayari kuwapeleka madaktari 500 kwenda kufanya kazi Kenya, katika hali ya kawaida CHADEMA inapenda wasomi wetu wapewe fursa za kufanya kazi popote duniani, ili wakaongeze ujuzi vile vile wakajihakikishie kipato lakini ni lazima tulifanye jambo hili wakati tukiwa na uhakika wa Usalama kwa wataalam wetu.
Mpaka sasa hivi tunao upungufu mkubwa wa madaktari lakini jana Waziri wa afya anamwambia Rais tunao madaktari wa kutosha na tunao madaktari hawana kazi kwa hiyo tunaweza kuwatoa madaktari wetu kwenda kufanya kazi Kenya kwa sababu hapa Tanzania hawana kazi.
CHADEMA tunasema kitu kimoja, madaktari Tanzania hawatoshi na tunao uhaba mkubwa wa madaktari ni vyema Serikali ikasema haina uwezo wa kuwalipa madaktari lakini isiseme inao madaktari wa kutosha.
Kwa mujibu wa viwango wa shirika la afya duniani WHO kwa nchi kama Tanzania inatakiwa iwe na daktari mmoja kwa watu 10,000, kwa takwimu za sasa daktari mmoja wa Tanzania anahudumia wananchi elfu ishirini na nane (28,000), kwa viwango vya WHO ni daktari mmoja kwa watu elfu kumi (10,000), wenzetu Wakenya wameshafikia viwango vya WHO, daktari mmoja anahudumia wagonjwa elfu nane (8,000).
Kinachotokea Kenya ni kwamba madaktari wamegoma, ili wapate maslahi bora nchini mwao, wanashinikiza ifuatwe Katiba nchini mwao, wanashinikiza Serikali yao itambue mfumo bora wa kutoa huduma ya afya katika Taifa lao, kimatibabu Wakenya wako mbali sana ukilinganisha na Tanzania.
Lakini sisi ambao ndo wagonjwa, sisi ambao ndo masikini, tuko tayari tuwatoe madaktari wetu wakazibe pengo ambalo limeachwa na madaktari waliogoma Kenya, ukienda kwenye mitandao ya kimataifa jana na leo Watanzania tunadhalilishwa, tunatukanwa na madaktari wa Kenya tunatukanwa na Wakenya kwamba tunakwenda kuingilia mambo ya ndani ya nchi yao,na wanasema ngoja vijana wa Kitanzania waende nchini kwao wakatoe matibabu, wanaenda hatua mbali zaidi wanasema madaktari wa Watanzania wajapikwa vya kutosha, hawana utaalam wa kutosha wanakwenda kuua ndugu zao.
CHADEMA tunasema hivi, Rais Magufuli acha mchezo wa kucheza na maisha ya madaktari wetu, katika mazingira ya kawaida, ingekuwa wanakwenda Kenya wakati kuna hali ya utulivu, kuna hali ya uhakika wa Usalama Kenya tungeruhusu vijana wetu wakafanye kazi kwa sababu hata Wakenya ni ndugu zetu, lakini katika mazingira ambayo kuna mgomo Kenya, kuna kutoelewana kati ya Serikali ya Kenya na madaktari wao, sisi ndio tuwe kimbelembele cha kuwatoa watoto wetu kwenda kutibu Kenya wakati Wakenya wenyewe hawawataki? ni kuweka maisha ya Watanzania wenzetu, wataalam wetu katika hatari, sisi kama Chama Kikuu cha Upinzani tunapinga, na naomba Mkutano huu Mkuu wa Kanda ya Pwani utoe tamko la kupinga madaktari wetu kwenda nchini Kenya.
Magufuli na Serikali yake wawape ajira vijana wetu vituo vya afya havina madaktari, Sera yetu ya Taifa inasema vituo vyetu vya afya lazima vihudumiwe na madaktari lakini mpaka leo hakuna madaktari kwenye vituo vya afya kwa sababu Serikali imeshindwa kuajiri.
Kwa hiyo wapo vijana wengi kwa muda wa miaka miwili hawajaajiriwa lakini suluhu sio kuwakimbizia nchi za jirani ambazo zina migogoro na wataalam wao, suluhu ni Serikali yetu itafute fedha iwaajiri vijana hawa, mama zetu, wazee wetu, vijana wetu wanawahaitaji madaktari hawa wawatibu katika vituo vyetu vya afya katika zahanati zetu katika hospitali zetu, Kwa hiyo naomba Mkutano Mkuu Maalum wa Kanda Pwani, naomba mnikubalie Kama Mwenyekiti wa Chama kupitia Mkutano huu tutoe tamko hili rasmi la kupinga madaktari wetu kwenda nchini Kenya.

About Author
  • mwana habari Read More